
Katika hali ya kile kinachoonekana kuwa ni shambulizi la Kigaidi, zaidi ya Watu 80 wameuawa kwa kugongwa na kukanyagwa na gari na wengine kupigwa risasi.
Tukio hilo limetokea katika kitongoji cha Promenade de Anglals jijini Nice nchini Ufaransa mnamo majira ya saa 5 usiku sawa na saa 6 usiku kwa saa za Afika Mashariki, ambapo mamia ya watu walikuwa wamekusanyika kuangalia fataki kwenye kilele cha sikukuu ya Bastile.
Duru za kipolisi zinadai kuwa dereva mmoja ambaye hakujulikana uraia wake, alilivurumisha lori kwenye kundi hilo la watu akipita katikati yao takribani umbali wa kilomita 2 hivi, akiwagonga na kuwakanyaga na akiwafyatulia risasi wengine na kusababisha vifo hivyo kabla ya yeye kupigwa risasi na kuuawa na maofisa wa polisi.
Baada ya kumuua dereva huyo walifanya upekuzi kwenye gari hilo na kukuta kitambulisho kikionyesha kuwa alikuwa na umri wa miaka 31, Ufaransa-Tunisia.Pia ndani ya gari hiyo walikuta bunduki na silaha nyingine kali. Waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo Bernard Cazeneuve amesema kuwa watu 80 wamefariki na wengine 18 wako katika hali mbaya(mahututi).
Naye raisi wa nchi hiyo Francois Hollande akiongea kupitia Luninga ya nchi amesema tukio hilo ni la kigaidi na hali ya taadhari iliyotarajiwa kufikia kikomo mwishoni mwa mwezi huu itaongezwa kwa miezi mingine mitatu. Pia akaongeza kuwa Wanajeshi wataendelea kuwasaidia Polisi kudumisha ulinzi na kuwashauri raia wasalie majumbani.